Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban, Baraza la usalama walaani shambulio huko Mogadishu

Ban, Baraza la usalama walaani shambulio huko Mogadishu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na wajumbe wa Baraza la Usalama wamelaani vikali shambulio la Jumatanombele ya mgahawa wa Jazeera  huko Mogadishu nchini Somalia uliosababisha vifo na majeruhi. Katika taarifa zao zilizotolewa kwa nyakati tofauti, Bwana Ban na wajumbe hao wametuma risala za rambirambi kwa wafia wa shambulio hilo huku wakiwatakia ahueni ya haraka majeruhi. Wametoa shukrani kwa vikosi vya Ulinzi vya Somalia kwa vile walivyochukua hatua haraka baada ya tukio pamoja na vile vya Umoja wa Afrika nchini Somalia, AMISOM kwa Jinsi walivyowatia usaidizi.

Katibu Mkuu amesema Umoja wa mataifa umejizatiti kuhakikisha kusaidia serikali ya Somalia katika kuzuia mashambulizi ya aina hiyo na kuwawajibisha wahusika. Nao wajumbe wa baraza la usalama pamoja na kurejelea mshikamano na wananchi wa Somalia wamesema vitendo vya kigaidi haviwezi halalishwa kwa misingi yoyote ile na kwamba tukio hilo halitakwamisha azma ya wananchi ya kusonga mbele katika kujiletea amani ya kudumu na kuimaraisha taasisi zao za kitaifa.