Baraza la Usalama lalaani shambulizi la bomu Beirut

2 Januari 2014

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali shambulio la bomu lililotekelezwa leo Januari 2 kusini wa Beirut nchini Lebanon, na ambalo liliwaua watu wapatao 5 na kuwajeruhi wengine wengi. 

Wanachama hao wa Baraza la Usalama wametuma salamu za rambi rambi kwa familia za wahanga na kutoa pole zao kwa wote walojeruhiwa katika tukio hilo la kinyama, pamoja na watu na serikali ya Lebanon.

Wanachama hao wa Baraza la Usalama pia wamesisitiza kuwa ugaidi wa aina yoyote ile ni mojawapo ya tishio kubwa zaidi kwa amani na usalama wa kimataifa, na kwamba vitendo vyovyote vya kigaidi ni uhalifu na hiaviwezi kukubalika kwa misingi yoyote ile, bila kujali kichochezi, wapi unapofanyika au wakati na mtu anayeutekeleza.

Wamesisitiza pia haja ya kuwawajibisha wale wanaovitekeleza vitendo vivyo, na haja ya kukabiliana na ugaidi kwa vyovyote vile, chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa na majukumu yote ya sheria ya kimataifa.