Juhudi za kutokomeza ukeketaji zinaenda kwa mwendo wa pole: WHO

2 Januari 2014

Hatua za kutokomeza ukeketaji wa wanawake zimekuwa zikiendelea kwa mwendo wa pole sana, na juhudi zaidi zinahitajika katika ngazi za kisiasa na kijamii ili kutokomeza desturi hiyo. Hayo yamechapishwa kwenye jarida la Shirika la Afya Duniani, WHO, ambalo limesema wanawake wapatao milioni 125 walio hai wamepitia ukeketaji wa aina moja au nyingine. Wengi wa wanawake hao hupata madhara makubwa kimwili na kihisia.

Katika mataifa kama Djibouti, Misri na Somalia, asilimia 90 ya watoto wa kike hufanyiwa ukeketaji wa aina fulani, wengine wao hata wakiwa bado hawajafikisha umri wa kutembea.

Kufikia sasa, ni nchi chache zimepunguza viwango vya ukeketaji, zikiwemo Kenya ambayo imepunguza ukeketaji kutoka asilimia 38 mwaka 1998 hadi 26% mwaka 2008; na Jamhuri ya Afrika ya Kati, kutoka 43% mwaka 1994 hadi 24% mwaka 2010. Nchi nyingine barani Afrika hazijaona mabadiliko yoyote, huku nyingine zikizidi kuimarisha desturi hiyo mbaya inayowanyanyasa wanawake.