Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Sudan Kusini bado yanaendelea: UNMISS

Mapigano Sudan Kusini bado yanaendelea: UNMISS

Habari kutoka Sudan Kusini zinasema kuwa mapigano bado yanaendelea hususan jimbo la Unity na Jonglei. Afisa kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo UNMISS Joseph Contreras ameiambia Radio ya Umoja wa Mataifa kuwa mapigano hayo ni kwenye mji wa Mayone jimbo la Unity na kwenye viunga vya mji wa Bor huko Jonglei.

(Sauti ya Joseph)

“Kwa bahati mbaya mapigano hayajakoma Sudan Kusini licha ya Rais Salva Kiir Maryadit na makamu wake wa zamani Riek Machar wakubaliane kuanza mazungumzo leo huko mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa. Mapigano makali yaliripotiwa jana kwenye mji wa Mayome, jimbo la Unity, na mapigano mengine ya hapa na pale mji wa Bor.Kuhusu vifo, kwa wiki moja sasa tumekuwa tunakadiria idadi ya  watu elfu Moja, na  makadirio ya juu zaidi ya hapo ni lazima yafanyike kwa uangalifu.”

Bwana Contreras amesisitiza kuwa UNMISS inaona mzozo huo kuwa ni wa kisiasa zaidi katika kusaka madaraka ndani ya chama tawala cha SPLM.