Hali Sudan Kusini bado mbaya, mapigano yanaendelea

30 Disemba 2013

Hali ya usalama nchini Sudan Kusini bado ni mbaya kwani mapigano bado yanaendelea na idadi ya wanaosaka hifadhi kwenye ofisi za ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS imeongezeka hadi Elfu Sabini.

Hayo amesema Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Disemba Balozi Gerard Araud alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mkuu wa UNMISS Hilde Johnson na Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani ndani ya Umoja wa Mataifa Herve Ladsous.

 (Sauti ya Balozi Araud)

 “Kuna matukio mengi ya mapigano, mathalani huko Bor, mapigano kwenye mji wa Malakal kati ya jeshi la serikali na waasi, na huko mji wa Bentiu ambako kikosi cha serikali kimejiweka sawa kuutwaa. Kwa hiyo kwa sasa naweza kusema nchini kote kuna wakimbizi wa ndani Laki Moja na Elfu Themanini.”

Balozi Araud amesema kuwa kwa sasa ni vigumusanakuwa na idadi kamili ya waliouawa lakini akazungumzia pia uimarishaji wa UNMISS.

(Sauti ya Araud) 

“Kuhusu kuimarisha kikosi hicho, mambo  yanaenda vizuri na inaweza kukamilika wiki chache zijazo, na mjuavyo askari hao watatoka UNAMID, MINUSTAH, UNMIL na ONUCI na kutoka MONUSCO imekubaliwa angalau kuhamisha polisi lakini kuhusu kuhamisha kikosi cha askari uamuzi wa hilo bado kwa sasa.”

Balozi Araud aliulizwa kuhusu  ushiriki waUgandakwenye mzozo huo……

(Sauti ya Balozi Araud)

“Tunapaswa kukumbuka kuwa hakuna pande mbili, bali kuna serikali halali ambayo ni ile ya Rais Kiir na kuna waasi, na katika sheria ya kimataifa baraza la usalama halina kauli yoyote pindi serikali halali inapotaka kurejesha mamlaka kwenye eneo lake.”

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter