Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yasambaza vifaa vya kujikinga na baridi kali kwa wakimbizi wa Syria

UNHCR yasambaza vifaa vya kujikinga na baridi kali kwa wakimbizi wa Syria

Vifaa vya kujikinga na baridi kali vilivyosafirishwa kwa ndege hadi Kaskazini Mashariki mwa Syria wiki mbili zilizopita, sasa vimeanza kusambazwa kwa zaidi ya wananchi Elfu Hamsini walio kwenye mazingira hayo magumu. Vifaa hivyo vilisafirishwa kutoka Erbil, Uturuki ni pamoja na mablanketi ya kutia joto, mahema ya nailoni, vifaa vya jikoni na vinginevyo vya kujisafi.

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, nchini Syria Tarik Kurdi amesema kila siku wanasambaza kwa zaidi ya watu Elfu Mbili Mia Tano kwenye jimbo la Al HAssakeh na kwamba vifaa hivyo vitakuwa na usaidizi mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo ambao kwa miezi kadhaa walikosa msaada wa aina yoyote.

Usafirishaji wa vifaa hivyo kwa ndege unafuatia makubaliano kati ya serikali za Syria na Iraq ambapo hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kutumia eneo la Iraq kusambaza vifaa vya msaada Syria.