Ban, Baraza la Usalama walaani shambulio la kigaidi nchini Urusi

30 Disemba 2013

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio la kigaidi huko Volgograd nchini Urusi ambalo limesababisha vifo vya watu 16 na wengine wengi kujeruhiwa. Msemaji wa Umoja wa Mataifa amemkariri Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akisema yuko na mshikamano na wananchi wa Urusi wakati huu mgumu kutokana na shambulio hilo la kigaidi kwenye kituo cha treni. Ametuma salamu za rambi rambi kwa wafiwa na serikali ya Urusi huku akitaka wahusika wa tukio hilo la kikatili wafikishwe mbele ya sheria.

Wakati huo huo, wajumbe wa baraza la Usalama kupitia kwa Rais wake Balozi Gérard Araud wa Ufaransa wameshutumu vikali shambulio hilo wakisema ugaidi haukubali kwa misingi yoyote ile na kwamba vitendo vya aina hiyo ni tishio kwa usalama duniani. Wajumbe wametaka wahusika pamoja na wale wanaowafadhili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria huku wakisihi nchi zote kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimo ya baraza kutoa ushirikiano juu ya suala hilo.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter