Shambulio dhidi ya UNAMID, Ban alaani vikali, atuma rambirambi kwa wafiwa

30 Disemba 2013

Huko kwenye jimbo la Darfur, nchini Sudan watu wasiojulikana wameshambulia msafara wa kikosi cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wa kulinda amani kwenye eneo hilo, UNAMID na kusababisha vifo vya walinda amani wawili, mmoja kutoka Senegal na mwingine kutoka Jordan. Kutokana na ripoti hizo, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon ameshutumu vikali shambuli hilo huku akituma risala za rambirambi kwa familia za walinda amani hao na serikali ya Senegal na ile ya Jordan. Habari zinasema wakati UNAMID wanajibu shambulizi, mmoja wa waliotekeleza shambulio hilo aliuawa na mwingine amejeruhiwa.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban amesema ni matarajio yake kuwa serikali ya Sudan itawafikisha mbele ya sheria waliohusika na shambulio hilo na mengineyo ya awali dhidi ya kikosi cha UNAMID.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter