Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azungumzia mkwamo wa usafirishaji wa kifaa muhimu Syria

Ban azungumzia mkwamo wa usafirishaji wa kifaa muhimu Syria

Kufuatia taarifa ya kwamba usafirishaji wa kifaa muhimu cha silaha za kemikali Syria uliokuwa ukamilike tarehe 31 mwezi huu unaweza kupata mkwamo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesisitiza kuwa jitihada za kimataifa za kutokomeza mpango huo zinaendelea kama ilivyodhihirishwa na kufikiwa kwa malengo mengine katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Msemaji wa Umoja wa Mataifa amemkariri Bwana Ban akisema kuwa licha ya uwezekano wa kuchelewa kufikiwa kwa lengo hilo, tume ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na shirika la kimataifa la kutokomeza silaha za kemikali inaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali ya Syria na nchi nyinginezo zinazosaidia kuhakikisha mitambo na vifaa vinavyohusika na mpango wa silaha za kemikali, vinasafirishwa nje ya nchi hiyo kwa usalama mapema iwezekanavyo. Katibu Mkuu amempongeza Sigrid Kaag, mratibu wa tume hiyo pamoja na jopo lake kwa vile ambavyo wanafanya kazi yao kwa kasi na katika mazingira yenye changamoto.