Ofisi ya haki za binadamu yaelezea hofu yake kuhusu sheria inayopinga mapenzi ya jinsia moja Uganda

27 Disemba 2013

Ofisi ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, hii leo imeelezea hofu yake kufuatia kupitishwa kwa mswada wa sheria inayopinga mapenzi ya jinsia moja nchini Uganda mnamo Ijumaa ya tarehe 20 Disemba wiki ilopita. Sheria hiyo itaweka hukumu ya kifungo cha maisha kwa wapenzi wa jinsia moja na vifungo kwa wale wanaodhaniwa kuendeleza mwenendo huo. Jason Nyakundi na taarifa kamili

(TAARIFA YA JASON)

Katika taarifa ilotolewa leo, ofisi ya haki za binadamu imesema sheria hiyo itakuwa na madhara makubwa, siyo tu kwa haki za msingi za wapenzi wa jinsia moja, lakini pia kwa kazi ya watetezi wa haki za binadamu na juhudi za kukabiliana na virusi vya HIV na Ukimwi nchini.

Ofisi hiyo imesema wapenzi wa jinsia moja nchini Uganda ni kundi lililotelekezwa, na tayari wanatengwa na kunyanyapaliwa. Ofisi hiyo imesema ikiwa itatiwa saini na rais, ikisainiwa, sheria hiyo itaongeza ubaguzi na unyanyapaa, na kuhalalisha ubaguzi.

Imeongeza kuwa vipengee vya mswada huo vinakiuka dhahiri haki ya uhuru, faragha, kutobaguliwa, pamoja na kujieleza na kujumuika kama zinavyolindwa na mkataba wa Uganda na mkataba wa kimataifa kuhusu haki za umma na kisiasa, ambao Uganda imeridhia.

Ofisi hiyo imetoa wito kwa rais wa Uganda kulinda haki za binadamu na kutotia saini mswada huo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter