Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yasaidia vikosi vya serikali ya DRC kuwango’a waasi wa ADF

MONUSCO yasaidia vikosi vya serikali ya DRC kuwango’a waasi wa ADF

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO, umesema waasi kutoka kundi la Allied Democratic Forces, ADF kutoka Uganda walivamia ngome za jeshi la kitaifa la DRC, FARDC katika aneo la Beni na Kamango, mkoa wa Kivu ya Kaskazini, na kuzidhibiti ngome hizo kwa muda.

Wakati wa uvamizi huo, waasi hao wa ADF wanaripotiwa kuteketeza nyumba kadhaa huko Kamango na kuwateka nyara watu wapatao 50. Kwa msaada wa MONUSCO, jeshi la FARDC lilijibu shambulizi hilona kuweza tena kuzidhibiti ngome zake zote mwishoni mwa siku.

Kwa mujibu wa ripoti za awali, wanajeshi sita wa FARDC waliuawa na saba kujeruhiwa wakati wa operesheni hizo, huku idadi ya waasi wa ADF walouawa ikiwa haijulikani bado. Kumeripotiwa pia wahanga wa kiraia, watu saba wakiwa wamepoteza maisha yao, na watu wengine wapatao 150,000 kulazimika kuhama makwao na wengine wapatao 200,000 wakikimbilia Uganda. MONUSCO imesema itafanya kila iwezalo kutekeleza majukumu yakena kuyamaliza makundi yote yenye silaha ambayo hueneza hofu, vifo, na uharibifu katika maisha ya raia.