Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu huru wa UM walaani mashambulizi ya anga huko Yemen

Wataalamu huru wa UM walaani mashambulizi ya anga huko Yemen

Wataalamu huru wa Umoja wa Matiafa kuhusu haki za binadamu leo wameelezea wasiwasi wao kufuatia shambulio la anga lililofanywa hivi maajuzi na ndege zisizo na rubani huko Yemen na kusababisha maafa kwa raia.

Yadaiwa kuwa mashambulizi yanayotumia ndege hizo zinazoweza kusababisha maafa yalifanywa na vikosi vya Marekani.

Kulingana na maafisa wa usalama raia 16 waliuawa na wengine 10 kujeruhiwa wakati misafara miwili ya watu waliokuwa wanatoka kwenye sherehe ya harusi ilipolengwa tarehe 12 mwezi huu huko Al-Baida wakidhaniwa kuwa ni wafuasi wa Al-Qaeda.

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya masuala ya mauaji kinyume na Sheria Christof Heyns amesema iwapo ndege hizo ni lazima zitumike, basi sheria za kimataifa za haki za binadamu zinapaswa kuzingatiwa na yapaswa kuwekwa bayana misingi ya kisheria ya matumzii yake.

Kwa upande wake Mtaalam Maalum juu ya mateso Juan Méndez pia alionyesha wasiwasi wake kuhusu uhalali wa mashambulizi ya angani  , akielezea kwamba kila nchi inalazimika kuchunguza matukio hayo na athari zake kwa raia. amesema mashambulizi haramu ni sawa na ukatili, unyama au udhalilishaji na katika mashambulio ya huko Al-Baida raia wamepata athari za kifikra na ni raia wasiokuwa na hatia.

Wametaka Marekani na Yemen kuchunguza na kubaini nani alihusika, na ni vigezo gani vilitumika kulenga raia na idadi ya waliouawa na iwapo wana mpango wa kufidia familia za waathirika wa tukio hilo.