Somalia kamilisha mipango kuhusu haki za binadamu: Mtaalamu UM

26 Disemba 2013

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya hali ya haki za binadamu nchini Somalia Shamsul Bari hii leo ameitaka serikali ya Somalia kukamilisha na pia kutekelza mpango wa amani kuhusu haki za binadamu uliozinduliwa na baraza la mawaziri mwezi Agosti. Taarifa zaidi na Jason Nyakundi.

(Taarifa ya Jason)

Bwana Bari amesema kuwa mpango huo wa amani unaeleza kuhusu majukumu ya serikali na malengo yanayotarajiwa kuafikiwa katika muda mfupi na kukamilika kwake ni ishara ya kujitolea kwa serikali katika kuhakisha kuwepo kwa haki za binadamu nchini Somalia

Wito wa Bari unajiri baada ya bunge la Somalia kumthibitisha Abdiweli Sheikh Ahmed ambaye aliteuliwa na rais Hassan Sheikh Moahamud kuwa waziri mkuu mpya.

Mpango huo uliopendekezwa na bwana Mario kwa utawala wa Somalia umeegemea zaidi masuala ya haki za binadamu yanayohitaji kutekelezwa na kila wizara.

Mtaalamu huyo amesema kuwa mpango huo wa haki za binadamu unatoa fursa nzuri ya kunawiri kwa haki za binadamu nchini Somalia lakini hata hivyo ameongeza kuwa ikiwa hakuna kujitolea itakuwa vigumu kutekelezwa.