Baraza la Usalama lapitisha azimio la kuongeza vikosi vya amani Sudan Kusini

24 Disemba 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limepitisha azimio la kuongeza vikosi vya walinda amani wa UNMISS nchini Sudan Kusini, kufuatia ombi la Katibu Mkuu kwamba idadi ya vikosi hivyo iongezwe ili kuimarisha utoaji wa ulinzi kwa raia na huduma za kibinadamu, chini ya kipengee cha 7 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Barazahilolimeamua ya kwamba, kutokana na mazingira yaliyopo sasa nchini Sudan Kusini , UNMISS sasa itakuwa na idadi ya wanajeshi 12, 500, pamoja na kikosi cha askari polisi 1, 323 ikiwa ni nyongeza ya askari 5,500 na polisi 440.

Pia wanachama wa Barazahilowamemtaka Katibu Mkuu kuwasilisha ripoti kwa Baraza la Usalama katika kipindi cha siku kumi na tano kuhusu hatua zilizochukuliwa kutekeleza azimiohilo.  Baraza la Usalama ambalo limelaani vikali machafuko hayo,  pia limezitaka pande zote katika mzozo huo wa Sudan Kusini kusitisha mapigano mara moja, na kuanza mazungumzo ya amani, pamoja na kushirikiana na UNMISS wakati inapotekeleza majukumu yake ya kuwalinda raia. Wamesema pia mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa hayakubaliki.

Mara baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon alitoa shukrani kwa Baraza la Usalama kwa kuchukua hatua haraka na kusema kuwa pamoja na kuimarisha uwezo wa UNMISS, anaendelea na mazungumzo na viongozi wa kikanda ili kuhakikisha suluhisho la kisiasa kwa mzozo huo. Bwana Ban amesema hali bado si shwari, maelfu ya watu wamekimbia na raia wasio na hatia wanakuwa ni walengwa kutokana na makabilayao. Hivyo ametoa wito..

(Sauti ya Ban)

 “Napongeza uharaka na uamuzi wa pamoja wa wajumbe baraza la usalama hii leo. Naamini kwamba baraza na wajumbe wataendelea kutekeleza wajibu wao ili kuweza kutoa michango yao ya  vifaa na uwezeshaji mwingine unaotakiwa ili askari  hao waweze kujumuika ndani ya muda unaotakiwa. Bila hivyo sekretarieti ya Umoja wa Mataifa haitaweza kupeleka askari hao wa nyongeza kadri ianvyotakiwa. Lakini hata pamoja na usaidizi wote wa vifaa na kuimarisha UNMISS, uwezo wa kulinda raia hauwezi kufanyika.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter