Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa Umoja wa Mataifa wasikitikia ghasia kuenea na kuwalenga raia Sudan Kusini

Wataalam wa Umoja wa Mataifa wasikitikia ghasia kuenea na kuwalenga raia Sudan Kusini

Washauri maalum wa Umoja wa Mataifa wameelezea hofu yao kuhusu kulengwa kwa raia katika mapigano  ambayo yameanza kufuata mkondo wa ghasia za kikabila nchini Sudan Kusini.

Wahauri hao wa Katibu Mkuu ambao ni Adama Dieng anayehusika na kuzuia mauaji ya kimbari, Jennifer Welsh anayehusika na wajibu wa kulinda, wameonya kuwa mashambulizi yanayowalenga raia na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kama yale yalotekelezwa Juba na Jonglei, yanatosha kuitwa uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Tangu kujipatia uhuru mnamo mwaka 2011, Sudan Kusini imekumbwa na ghasia za kikabila na mashamulizi ya kulipiza kisasi yanayohusishwa na kuzozania uongozi wa kisiasa.

Washauri hao maalum wametoa wito kwa pande zote zinazozozana kujizuia na kuheshimu sheria za kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu. Wamewaomba hususan viongozi wenye ushawishi kutoa ujumbe dhahiri wa kuzuia mashambulizi dhidi ya watu au makundi ya watu kwa misingi ya kikabila.