Hatuondoki Sudan Kusini licha ya changamoto za kiusalama: Bi. Johnson

24 Disemba 2013

Hatutaondoka Sudan Kusini,  tupo hapa na tutaendelea kujiimarisha kwa maslahi ya wananchi, ni kauli ya Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, Hilde Johnson alipozungumza na waandishi wa habari mjini Juba, ikiwa ni zaidi ya wiki moja tangu mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaanze nchini humo.

Amesema wameshuhudia kupanuka kwa mgogoro, raia wanakimbia na wengine wanahama nchi hiyo na ili waweze kutekeleza jukumu lao la kulinda raia wametuma ujumbe mzito makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjiniNew York, ili waongezewe rasilimali watu na vifaa.

Bi Johnson amesema jibu walilopokea ni chanya kwani baraza la usalama linakutana Jumanne jioni kujadili pendekezo la katibu Mkuu la kuimarisha ujumbe wake Sudan Kusini, kwa askari, vifaa vya anga ili kuweza kulinda raia.

Amesisitiza kuwa mzozo wa Sudan Kusini ni wa kisiasa na hivyo utatatuliwa kisiasa na kwamba hakuna suluhu la kijeshi kwenye mzozo huo. Bi. Jonhson amesema kuna pande nyingi zinataka kutumia mzozo wa sasa kuendeleza ajenda zao lakini kimsingi mzozo wa sasa ni wa madaraka.