UNHCR yachukua hatua za kusaidia wale waliohama makwao kwenye Jamhuri ya Afrika ya Kati

24 Disemba 2013

Huku makabiliano ya kijamii yakiendelea sehemu kadha za Jamhuri ya Afrika ya kati, shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR  lina wasi wasi mkubwa kuhusu masuala ya usalama pamoja na ya kibinadamu kwenye maeneo yanayowahifadhi idadi kubwa ya watu waliohama makwao. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

 (Taarifa ya Assumpta)

Zaidi ya watu 710,000 wamelazimika kuhama makwao ndani mwa nchi tangu kuanza kwa mzozo mwaka mmoja uliopita. Wakristo wengi wametafuta hifadhi kwenye shule, makanisa na kwenye uwanja wa ndege huku waislamu wakiishi na familia zingine.

Wakati mapigano kati ya makundi yaliyojihami yakiwa yameendelea tangu mwezi Disemba,nayo mapigano ya kijamii kwenye mji mkuu Bangui yamekuwa yakiendela tangu mapema mwezi huu.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Jamhuri ya Afrika ya kati Lasare Kouassi Etien anasema kuwa hofu iliyopo kwa sasa ni kuendelea kuzoroteka kwa hali kibinadamu na usalama kwenye maeneo waliko wakimbizi wa ndani. Hata hivyo amesema viongozi wa madhehebu ya kikristo na kiislamu wanaendelea kuelimisha wananchi katika kambi za wakimbizi wa ndani umuhimu wa kustahimiliana.

UNHCR tayari imesambaza mahema, matandiko ya kulalia, neti za mbu , mablanketi na  nguo. Lakini kulingana na tathmini ya hivi majuzi  iliyofanyiwa wakimbizi wa ndani mahitaji bado ni makubwa.