Misaada yawafikia maelfu watu walioathiriwa na ghasia nchini Sudan kusini

23 Disemba 2013

Mashirika ya utoaji misaada yamechukua hatua za kuwahudumia maelfu ya raia walioathiriwa na mizozo inayolikumba taifa la Sudan Kusini wakiwemo watu 20,000 walio kwenye makao ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa mjini Juba. Jason Nyakundi na taarifa kamili.

(Taarifa ya Jason Nayakundi)

Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na yale ya Umoja wa Mataifa yanatoa huduma za kuokoa maisha kwenye vituo viwili zikiwemo huduma za maji na usafi, makao na huduma za afya za dharura kwa watu waliolazimika kuhama makwao kutokana na ghasia.

Vyoo vya dharura vinachimbwa, huku biskuti za lishe ya juu zikisambazwa pamoja na huduma za ugavi wa  vifaa vinavyotumiwa katika matibabu kwenye hospitali za mji wa Juba. Mashirika ya utoaji misaada yamefanikiwa kupeleka chakula kwa watu 7000 ambao wametafuta hifadhi kwenye makao ya Umoja wa Mataifa eneo la Bentiu.

Hali inatajwa kuwa ngumu kwenye majimbo ya Jonglei na Unity ambapo mapigano yamewalazimu maelfu ya watu kuhama makwao. Kumekuwa na ripoti za kuvunja moyo zikiwemo za watoto waliotenganishwa na wazazi wao huku watoa huduma za kibinadamu wakikabiliwa na wakati mgumu baada ya visa vya kuporwa kwa makao ya mashirika ya utoaji huduma za kibinadamu.