Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS kuimarisha uwepo wake Unity na Jonglei; Ban ataka wanasiasa Sudan Kusini kuchukua hatua

UNMISS kuimarisha uwepo wake Unity na Jonglei; Ban ataka wanasiasa Sudan Kusini kuchukua hatua

Wakati hali ya amani inazidi kuzua sintofahamu huko Sudan Kusini, Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Hilde Johnson ametoa taarifa akithibitisha mipango ya Umoja huo ya kuimarisha uwepo wa vikosi vyake kwenye maeneo ya Bor jimbo la jonglei na Pariang jimbo la Unity. Bi. Johnson amesema azma ya ujumbe wa umoja wa mataifa nchini Sudan UNMISS ambao yeye anaongoza, ni kulinda raia na kwamba kamwe hawatatishika na vitisho au  vikwazo vyovyote vinavyowekwa dhidi yao. Hatua ya Umoja wa Mataifa kulinda raia iko bayana kwenye vituo vyake nchini Sudan Kusini ambako hadi sasa wananchi wapatao Elfu 40 wamesaka hifadhi ili kukwepa mapigano yaliyoanza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Tayari UNMISS imeondoa wafanyakazi wasio wa lazima na kutoka Bor kwenda Juba huku wale wasiohitajika Juba wakipelekwa Entebbe, Uganda. Mkuu huyo wa UNMISS hata hivyo amesisitiza kuwa kuondoka kwa wafanyakazi si kwamba wanaitelekeza Sudan Kusini bali wamechukua hatua hiyo ili kuhakikisha rasilimali chache zilizopo zinaelekezwa kwenye mahitaji zaidi.

Akizungumza mwishoni mwa ziara yake nchini Ufilipino, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema mzozo wa Sudan Kusini unazidi kuleta madhara kwa wananchi na amerejelea wito wake kwa pande zinazopingana kutumia meza ya mazungumzo kumaliza mzozo huo.