Kuzorota kwa usalama Sudan Kusini kwatia wasiwasi Baraza la Usalama

20 Disemba 2013

Kufuatia ripoti kuhusu kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama Sudan Kusini Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mashauriano ya dharura na faragha kuhusu hali nchini humo wakati huu ambapo imeripotiwa vifo vya raia 20 na walinda amani huko Akobo.

Rais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Disemba Balozi Gerard Araud kutoka Ufaransa amewaambia waandishi wa habari baada ya kikao hicho kuwa wajumbe wamesikitishwa na ripoti za kile kinachoendelea ikiwemo shambulizi kwenye kambi ya UNMISS tarehe 19 mwezi huu lililosababisha vifo vya raia 20 na walinda amani. Wametuma salamu za rambambi kwa wafiwa huku wakitoa maelekezo kwa viongozi..

(Sauti ya Balozi Araud)

“Wamemtaka Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar kuonyesha uongozi wao katika kumaliza mzozo huo haraka kwa amani na kutaka kusitishwa kwa chuki na kuanza mara moja kwa mashauriano. Wametaka pande zote kuhakikisha ulinzi kwa wanaoshikiliwa.”

Wamelaani mashambulizi yanayolenga raia kwa misingi yoyote ile ikiwemo ukabila pamoja na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi na hata miundombinu huku wakiunga mkono jitihada za mamlaka ya IGAD, Muungano wa Afrika, na Umoja wa Mataifa za kuweka mashauriano baina ya viongozi wakuu. Kuhusu usaidizi wa kibandamu, wajumbe wa baraza wamesema…

(Sauti Balozi Araud)

Wametaka pande zote kuruhusu upelekaji na usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwa wahitaji kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa Mataifa za usaidizi wa kibinadamu. Wameshutumu vikali mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta ambayo yamesababisha vifo vya wafanyakazi kwenye mitambo hiyo. Wametaka pande zote kuhakikisha usalama kwenye miunndombinu ya kiuchumi na usalama wa wafanyakazi.”

Wajumbe wamesisitiza azma yao ya kuendelea kufuatilia kwa karibu hali nchini Sudan Kusini na kuchukua hatua mahsusi iwapo itahitajika kufanya hivyo.