Raia 20 na walinda amani wauawa Sudan Kusini; Baraza la Usalama lakutana

20 Disemba 2013

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS, umethibitisha kuwa walinda amani wawili kutoka India waliuawa katika shambulizi la Akobo, na kwamba mlinda amani mwingine kutoka India amepelekwa kwa kituo cha matibabu cha UNMISS Malakal.

Katika taarifa yake, UNMISS imelaani vikali machafuko na ukatili uolotendeka Akobo na ambao unaendelea katika maeneo mengine nchini humo.

Imetoa wito kwa makundi husika kujiepusha na ghasia zaidi na kutafuta suluhu la amani kwa mzozo huo.

Joseph Contreras, ni kaimu msemaji wa UNMISS anasema hadi sasa raia 20 wameuawa kutokana na shambulio la Akobo na anasema kinachoendelea Juba.

(Sauti ya Joseph)

“Mji unazidi kutelekezwa,watu wanaondoka mjini Juba wakiwa kwenye mistari, maeneo mengi yako matupu, kuna uporaji mkubwa na makazi mengi  yamechomwa moto na kuna miili mingi ya watu imetapakaa kwenye mji huo mkuu.”

Wakati hayo yakiendelea Baraza la usalama leo limekuwa na mashauriano ya faragha kuhusu Sudan Kusini.