Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwendesha mashtaka ICC aomba kuahirishwa tarehe ya kesi dhidi ya Kenyatta

Mwendesha mashtaka ICC aomba kuahirishwa tarehe ya kesi dhidi ya Kenyatta

Mwendesha Mashtaka Mkuu katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC huko The Hague, Fatou Bensouda leo amewasilisha ombi la kutaka kusogezwa mbele tarehe ya kuanza kusikilizwa kesi dhidi ya Uhuru Kenyatta. Katika ombi hilo, Bensouda anasema kuwa uamuzi wake unazingatia suala la ushahidi kwa mujibu wa mkataba wa Roma.

Amesema katika miezi miwili iliyopita, mmoja wa shahidi muhimu upande wa mashtaka dhidi ya Kenyatta alidokeza kutokuwa tayari kutoa ushahidi. Na tarehe Nne mwezi huu, shahidi mwingine muhimu alikiri kutoa ushahidi wa uongo juu ya tukio moja muhimu kwenye kesi hiyo.

Mwendesha mashtaka huyo amesema kwa kuzingatia kujitoa kwa mashahidi hao wawili muhimu ameamua kesi iliyopo hivi sasa kwenye mahakama hiyo haikidhi vigezo vya ushahidi vinavyotakiwa kwa kesi kuweza kuanza kusikilizwa.

Kwa mantiki hiyo ameomba muda zaidi wa kusaka ushahidi na kuangalia iwapo ushahidi atakaopata utawezesha ofisi yake kukidhi vigezo vinavyotakiwa kwa kesi kusikilizwa.

Bi. Bensouda amesema azma yao ya kuhakikisha haki inapatikana kwa wahanga wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007 imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi huku akisisitiza kuwa uamuzi wake wa kuomba kuahirishwa kwa tarehe ya kuanza kusikilizwa kesi hiyo umefanyika kwa umakini.

Kesi dhidi ya Uhuru Kenyatta ilipangwa kuanza kusikilizwa tarehe Tano mwezi Februari mwakani.