Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yabainisha maeneo yanayohitaji msaada wa haraka CAR

WHO yabainisha maeneo yanayohitaji msaada wa haraka CAR

Timu ya wataalamu wa shirika la afya ulimwenguni WHO imetembelea kambi moja iliyoko karibu na uwanja wa  ndege wa Mpoko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kambi ambayo inahifadhi zaidi ya raia 45,000 waliokimbia machafuko yanayoendelea nchini humo.

Wataalamu hao wametembelea eneo hilokwa ajili ya kufanya tathmini juu ya mahitaji muhimu ya kiafya yanayopaswa kutilia kipaumbele. George Njogopa na ripoti kamili.

(Ripoti ya George)

WHO inasema kuwa kambi ya Mpoko kama ilivyo maeneo mengi nchini humo inakabiliwa na hali ngumu ya ukosefu wa huduma za kiafya na kwamba maelfu ya raia wanaishi kwenye mlundikano mkubwa huku wakikosa huduma za majisafi na salama.

Kuna wasiwasi kuwa hali hiyo huenda ikachochea kujitokeza kwa magonjwa ya mlipuko ikiwmeo kuhara, kipindupindu na taifodi.

Katika jitihada zake za kukwamua hali ya mambo WHO na washirika wake inaona haja ya kutolewa huduma za haraka kamavile kutoa upasuaji kwa wale waliojeruhiwa, kurejesha katika hali ya kawaida vituo vya kiafya vilivyoharibika na kusambaza madawa kwenye vituo hivyo.

Timu hiyo ya wataalamu pia imetoa mwito wa kuratibiwa shughuli za kiafya ikiwemo kupanua uwigo wa maeneo yanayofikiwa na huduma hizo za kiafya.