Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya madaktari Somalia, Mjumbe wa UM alaani vikali

Mauaji ya madaktari Somalia, Mjumbe wa UM alaani vikali

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Nicholas Kay ameshutumu vikali shambulio la hii leo nje kidogo ya mji mkuu Mogadishu, lililolenga msafara uliokuwa ukielekea kituo kimoja cha afya.

Bwana Kay amesema kwenye shambulio hilo lililofanywa na watu wasiofahamika waliokuwa wamejihami, watu sita wameuawa wakiwemo madaktari wanne mmoja ni raia wa Somalia na watatu wa Syria pamoja na mlinzi na dereva. Halikadhalika abiria wawili wamejeruhiwa.

Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu amelaani kitendo hicho ambacho amesema kimetokea wakati Somalia ikitegemea zaidi taasisi za kiraia na matabibu wa afya wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu kurejesha huduma za afya.

Ameshutumu wale wanaokwamisha jitihada hizo za serikali na jamii ya kimataifa na kuitaka serikali ya Somalia kuchunguza tukio hilo na wahusika wafikishwe mbele ya sheria. Bwana Kay pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliofariki dunia na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi.