Baraza la Usalama lajadili ulanguzi wa madawa na amani na usalama Afrika Magharibi

18 Disemba 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadili amani na usalama barani Afrika, hususan suala la ulanguzi wa madawa ya kulevya eneo la Sahel na Afrika Magharibi.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema kote duniani, ulanguzi wa madawa ya kulevya na uhalifu wa kimataifa wa kupangwa hutishia usalama, kudunisha uongozi wa kisheria, na kutishia usalama na utulivu

 (SAUTI YA BAN)

“Katika nchi nyingi, mitandao ya uhalifu wa kupangwa pia huchangia vitendo vya kigaidi na makundi yenye misimamo mikali. Ufisadi, mipaka isodhibitiwa vyema na uhaba wa rasilmali na ushirikiano, huchangia hata zaidi tatizo hili. Kwa sababu ya mitandao ya ulanguzi wa madawa na mbinu zao zinazobadilika, ni lazima tuendeleze uelewa wetu ili kutafuta njia bora za kukabiliana nao. Tunakabiliana na changamoto kubwa Afrika Magharibi na eneo la Sahel”

 Akizungumza baada ya Katibu Mkuu, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na madawa ya kulevya na uhalifu wa kupangwa, Yury Fedotov amesema kulingana na ripoti ya ofisi ya UNODC, suala la madawa ya kulevya Afrika Magharibi ni lenye kutia hofu.

 (SAUTI YA FEDOTOV)

 “Mihadarati hupitia eneo hilo, kwenda kwenye masoko ya faida. Fedha zitokanazo na biashara hii husaidia makundi ya uhalifu kuendeleza operesheni zao, na kusaidia vitendo vya kigaidi katika eneo. Tatizo la matumizi ya madawa limeongeza na pia kuchangia matatizo kama kuongezeka maambukizi ya HIV kwa sababu ya kudunga madawa.”

Baadaye, Bwana Ban pia amewahutubia waandishi wa habari, hali Sudan Kusini ikimulikwa.

(SAUTI YA BAN)

 “Nasikitishwa sana na hali inayoendelea sasa Sudan Kusini. Nimezungumza na Rais Salvar Kiir jana asubuhi kufanya kila awezalo kuhakikisha kumaliza machafuko. Huu ni mzozo wa kisiasa, na unahitaji kutatuliwa kwa dharura kupitia mazungumzo ya kisiasa. Kuna tishio la ghasia hizi kusambaa hadi majimbo mengine. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini umepokea ripoti za kuuawa watu wengi. Tunaendelea kuthibitisha ripoti hizi. Natoa wito kwa serikali kushirikiana kikamilifu na UNMISS wakati ikitekeleza majukumu yake ya ulinzi”