Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti kuhusu silaha za kemikali Syria iliibua mzozo barazani: Balozi Araud

Ripoti kuhusu silaha za kemikali Syria iliibua mzozo barazani: Balozi Araud

Rais wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Disemba Balozi Gerard Araud wa Ufaransa amewaeleza waandishi wa habari kuwa ripoti iliyowasilishwa na Katibu Mkuu Ban Ki-Moon ya uchunguzi wa silaha za kemikali nchini Syria iliibua mjadala mkali badina ya wajumbe wa baraza hilo.

Amesema ripoti hiyo ilieleza bayana kuwa silaha za kemikali zilitumika na kwamba wajumbe hawakujadili nani anawajibika na kitendo hicho lakini wao pamoja na Bwana Ban wamelaani na kutaka wahusika wafikishwe mbele ya sheria. Balozi Araud akaulizwa iwapo barazani walijadili nani alitumia silaha za kemikali huko Ghouta na Khan Al Assal nchiniSyria…

(Sauti  ya Balozi Araud)

“Tumekuwa na kikao kuhusu ripoti ya Sellstrom, kwa hiyo tumekuwa tukijadili ripoti hiyo. Sasa kuhusu Khan Al Assal, suala ni kwamba ujumbe ulifikia maafikiano na serikali ya Syria baada ya muda mrefu yaani miezi mitatu au minne baada ya shambulio la Khan Al Assal, na pia katika hali yoyote hali ya usalama haikuwa inaruhusu ujumbe kuelekea eneo Khan Al Assal.  Kuhusu nani anawajibika, suala hilo liliibuliwa na mjumbe mmoja na kusababisha vile unavyoweza kudhania, mvutano mkubwa usio wa kirafiki na mjadala ambao haukumalizika.”

Uchunguzi huo ulifanywa na jopo lililoongozwa na Profesa Ake Sellstrom ambaye pia alishiriki kwenye mashauriano ya leo kwa mujibu wa azimio namba 2118 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la mwezi Septemba mwaka huu.