Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado hali nchini CAR ni tete, mkutano maalum haukwepeki - Balozi Samba

Bado hali nchini CAR ni tete, mkutano maalum haukwepeki - Balozi Samba

Balozi wa kudumu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR katika Umoja wa Mataifa Léopold Ismael Samba amesema licha ya majeshi ya Ufaransa kusaidia katika kurejesha utulivu nchini humo bado mgogoro unafukuta na kwamba taifa hilo linakabiliana na changamoto na bado safari kuondokana na mgogoro huo ni ndefu.

Akizungumza katika mkutano wa baraza la haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa balozi Samba amesema kutokana na hali hiyo Jamhuri ya Afrika ya Kati inahitaji msaada kwa ajili ya mkutano maalum mwezi January mwakani pamoja na kupeleka wataalamu huru ambao amesema ni muhimu katika kuchagiza kuwajibishwa kwa watu waliohusika katika ghasia na ambao walikiri kuhusika.

Akizungumza kwa niaba ya kundi la Afrika msemaji wa Ethiopia Dk Tekeda Alemu amesema wanalaani vikali kuenea kwa uvunjaji wa haki za binadamu na sheria za kitu za kimataifa nchini CAR. Kadhalika ameitaka jumuiya ya kimataifa kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu nchini CAR na umuhimu wa kuwa na mkutano mwanzoni mwa mwaka 2014 kujadili hali ilivyozorota CAR.

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya EU, na Ufaransa zimesisitiza umuhimu wa kuwa na mkutano wa dharura mapema mwakani na kuharakishwa kwa uteuzi wa watalaamu huru kama ilivyoamuliwa na baraza kuu katika mkutano wake wa mwisho.