Shambulio dhidi ya MINUSMA; Ban, Baraza la Usalama walaani vikali

15 Disemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali shambulio dhidi ya vikosi vya kulinda amani na kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, lililotokea Jumamosi huko Kidali na kusababisha vifo vya walinda amani wawili kutoka Senegal na wengine saba kujeruhiwa wakiwemo askari wa jeshi la Mali.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Bwana Ban akitaka wahusika kufikishwa mbele ya mkono wa sheria na kusema kuwa Umoja wa Mataifa umejizatiti kuendeleza jukumu lake la usaidizi kwa wananchi wa Mali ili waweze kupata amani ya kudumu. Amewataka wananchi kukataa ghasia na kuunga mkono mchakato wa amani ikiwemo kushiriki katika awamu ya pili ya uchaguzi wa wabunge Jumapili.

Halikadalika Bwana Ban ametumba risala za rambirambi kwa serikali ya Senegal na familia za walinda amani wa Senegal waliopoteza maisha na kutakia ahueni ya haraka majeruhi. Wakati huo huo wajumbe wa Baraza la Usalama nao katika taarifa yao wameeleza kusikitishwa na shambulio hilo na kusema kuwa hakuna jambo lolote linaloweza kuhalalisha kitendo hicho. Wamesema wako na mshikamano na wananchi wa Mali, MINUSMA na vikosi vya Ufaransa vilivyoko nchini humo kuweka utulivu  na kwamba wahusika wafikishwe kwenye mkono wa sheria.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter