Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ahutubia Baraza la Usalama kuhusu ripoti ya silaha za kemikali Syria

Ban ahutubia Baraza la Usalama kuhusu ripoti ya silaha za kemikali Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, leo amelihutubia Baraza Kuu kuhusu ripoti ya uchunguzi katika madai ya matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria, kufuatia kukabidhiwa ripoti hiyo hapo jana na Profesa Åke Sellström, ambaye aliiongoza timu ya uchunguzi huo.

Ripoti hiyo inajumuisha matokeo ya uchunguzi wote wa timu hiyo katika matukio yote yalioripotiwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa tangu mwezi Machi mwaka huu 2013, pamoja na matokeo ya ziara yake Syria kati ya tarehe 25 na 29 Septemba.

Miezi mitatu iliopita, timu hiyo ilihitimisha kuwa, silaha za kemikali zilitumiwa kwa kiwango kikubwa mnamo Agosti 21, katika mtaa wa Ghouta mjini Damascus, na kusababisha vifo na madhara mengine hususan kwa raia.

 “Leo, naeleza kwa masikitiko makubwa kuwa timu hiyo ilikusanya ushahidi na maelezo ya kuthibitisha madai kwamba silaha za kemikali zilitumiwa mara kadhaa katika sehemu mbalimbali, dhidi ya raia na dhidi ya wanajeshi. Ingawa timu hiyo haikuweza kuthibitisha kila kinachohusika na madai hayo, tathmini yake ni kwamba silaha za kemikali huenda zilitumika mnamo Machi 19 Khan Al Asal, Agosti 24 Jobar na Aprili 29 Saraqueb na Agosti 25 Ashrafiah Sahnaya”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika uchunguzi wa matukio mawili ya matumizi ya silaha hizo, dalili za vipimo zilionyesha kuwa kemikali ya Sarin ilitumiwa. Bwana Ban amelaani vikali vitendo hvyo..

“Tunapozingatia suala la silaha za kemikali, jamii ya kimataifa huongea kwa sauti moja: matumizi yoyote ya silaha za kemikali, na mtu yeyote yule, katika mazingira yoyote yale, ni ukiukwaji mkubwa wa mkataba wa 1925 na vipengee vingine husika vya sheria ya kimataifa. Nalaani vikali mno matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria kama kosa dhidi ya maadili ya ubinadamu kwa ujumla”

Bwana Ban amesema jamii ya kimataifa ina wajibu wa kimaadili na kisiasa kuhakikisha kuwa walotumia silaha hizo wanawajibishwa, ili kuzuia matumizi yake siku zijazo, na kuhakikisha kuwa silaha za kemikali daima haziibuki kama kitu kinachotumiwa katika vita.

Ameelezea furaha yake kuwa tangu matukio ya Ghouta, jamii ya kimataifa imeweka nguvu pamoja kuhakikisha silaha hizo zinateketezwa nchini Syria, na sasa viwanda vyote vya kuzalisha silaha za kemikali vimeharibiwa.