Baraza la Usalama latakiwa kuchukua hatua kulinda waandishi wa habari mashakani

13 Disemba 2013

Baraza la usalama leo limeelezwa bayana madhila wanayokumbana nayo waandishi wa habari pindi wanapotekeleza majukumu yao na limetakiwa kuchukua hatua kuhakikisha wanalindwa dhidi ya vitendo hivyo.

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, Frank La Rue amelimbia baraza hilo wakati wa kikao maalum kuhusu ulinzi wa waandishi wa habari kuwa kila uchao watendaji hao hasa wanaotekeleza majukumu yao kwenye maeneo ya vita na mizozo, wanakabiliwa na vitendo vya mateso na hata kuuawa.

Amewaeleza wajumbe wakati wa kikao hicho cha faragha kuwa bila kuweka mfumo stahili dhidi ya vitendo hivyo na hata kuondosha ukwepaji sheria kwa wale wanaofanya vitendo hivyo, itakuwa vigumu sana kuwa na hakikisho la usalama wa waandishi wa  habari.

Bwana La Rue amesema matukio mengi ya ghasia dhidi ya waandishi wa habari hayachunguzwi na wale wanaohusika hawawekwi hadharani, hawafunguliwi mashtaka wala kuhukumiwa.

Ametolea mfano nchini Syria ambako waandishi wa habari 84 wameuawa tangu kuanza kwa mzozo huo mwezi Machi mwaka 2011 na huko Mali mwezi uliopita waandishi wawili wa habari waliuawa.

Baada ya kikao hicho, Rais wa baraza la usalama Balozi Gerard Araud wa Ufaransa akawaeleza waandishi wa habari kuwa kilikuwa cha manufaa.

(Sauti ya Balozi Araud)