Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aweka bayana mshikamano na wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Ban aweka bayana mshikamano na wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Salaamu, mimi ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.. ndivyo alivyoanza Bwana Ban ujumbe wake kwa watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, wakati huu ambapo ghasia zinaendelea nchini humo huko na kuweka maisha ya wananchi hatarini.

Ujumbe huo kwa njia ya radio ni takribani dakika mbili ambapo Katibu Mkuu ameamua kuzungumza moja kwa moja na wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, akiwasihi..

(Sauti ya Ban)

“Namsihi kila mmoja wenu kufuata njia ya amani. Umwagaji damu lazima usimame! Msiruhusu mbegu ya chuki kupandwa ili kuwagawa katika maeneo ambayo awali hakukuwa na mgawanyiko. Bila kujali imani ya dini, nyote mna historia moja na mustakhbali mmoja! Nawasihi viongozi wa kijamii, dini.. Waislamu na wakristo kuwa wajumbe wa amani. Nasihi mamlaka za mpito kulinda wananchi na kuzuia mzozo zaidi.”

Katibu Mkuu akatoa angalizo…

(Sauti ya Ban)

“Ujumbe wangu uko bayana kwa wale wote wanaofanya mauaji na uhalifu wa kibinadamu. Dunia inatizama na mtawajibishwa.”

Mwishoni akadhihirisha mshikamano, wakati huu wa hali ngumu..

(Sauti ya Ban)

 “Hamko peke yenu! Hatutawatelekeza. Vikosi vya Afrika na Ufaransa tayari viko nchini humo kuleta mabadiliko. Vikosi zaidi vitawasili haraka iwezekanavyo kurejesha utulivu. Tunajitahidi kuwapatia chakula, malazi na dawa. Na bado tuko pamoja nanyi kujenga amnai ya kudumu na mustakhbali bora kwenu nyote.”