CERF ni mkombozi wa wahitaji, twaomba mchangie kuokoa wahitaji: Ban

13 Disemba 2013

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa masuala ya usaidizi wa kibinadamu, OCHA leo imeandaa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF mjini New York. Assumpta Massoi amefuatilia mkutano huo na hii hapa ni ripoti yake.

(Ripoti ya Assumpta)

Mwaka huu pekee CERF ilitoa zaidi ya dola Milioni 82 kwa ajili ya shughuli za usaidizi wa kibinadamu nchini Syria, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika hotuba yake kwenye mkutano huo wa kuomba usaidizi zaidi kwenye mfuko huo. Amesema CERF umekuwa umekuwa mkombozi na nuru kwa wengi wenye uhitaji na walio hatarini duniani kote kuanzia Asia, Afrika na Mashariki ya Kati.

(Sauti ya Ban)

Mwaka huu mfuko wa CERF umeokoa watoto dhidi ya kutumikishwa na vikundi vyenye silaha nchini Mali. Uliwezesha wakimbizi Elfu 32 wa Somalia kurejea nyumbani. Wengi walio hatarini wanategemea msaada wenu ili kazi hii iweze kuendelea. Ndio maana nawaomba usaidizi zaidi kwa mfuko huu .”

Ban amesema mwaka huu pekee wahisani wamechangia dola Milioni 435 karibu lengo la dola Milioni 450. Hata hivyo amewasihi kuongeza usaidizi mwakani huku akitoa ahadi..

Ahadi yetu, ahadi yangu tutatumia kwa ufanisi mchango wenu. Tunafahamu fedha zinapatikana kwa ugumu. Tunawashukuru kwa kujitoa kwenu na kutuamini. Tunaahidi kuwa matumizi yake yatakuwa ya uwajibikaji na ya uwazi.”