Visa vya ugonjwa wa saratani vyafikia zaidi ya Milioni 14 duniani kote: IARC

12 Disemba 2013

Shirika la kimataifa la utafiti wa ugonjwa wa saratani,  IARC lenye uhusiano na lile la afya duniani, WHO leo limetoa takwimu mpya kuhusu ugonjwa huo zinazoonyesha ongezeko la wagonjwa. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Zaidi ya watu Milioni 14 walipoteza maisha mwaka jana kutokana na ugonjwa wa saratani ambapo aina za saratani zilizotajwa na ripoti hiyo kusababisha vifo zaidi ni ile ya mapafu, ini na tumbo. IARC inasema kuwa aina hizo za saratani ni miongoni mwa aina 28 ambazo zinaweka picha halisi ya mwelekeo wa kuongezeka kwa tishio la ugonjwa huo duniani kutokana na utafiti katika nchi 184 zilizofikiwa na utafiti huo huku saratani ya titi ikionekana kujitokeza zaidi pindi wagonjwa wanapojitokeza kwa uchunguzi. Dokta Christopher Wild, ni Mkurugenzi wa IARC

(Sauti ya Dkt. Wild)

 Nilipoangalia hizi takwimu mara ya kwanza nilishushwa sana na mwelekeo wa saratani miongoni mwa wanawake, hususan kwenye nchi za kipato cha chini na kati! Na suala kwamba saratani ya titi kwa sasa imeenea duniani kote, jambo ambalo zamani ugonjwa huu ulikuwa ni kwa nchi zilizoendelea!Lakini pia saratani  ya kizazi, ugonjwa ambao zamani ulipatikana zaidi nchi tajiri na sasa unadhibitiwa, lakini sasa unasababisha vifo zaidi miongoni mwa wasichana kwenye nchi zinazoendelea.”

 Dokta Wild anasema kuwa kilichothibitika sasa ni kwamba ugonjwa wa saratani siyo tena suala la nchi tajiri pekee bali nchi maskini pia lakini tofauti ni kwenye uwezo wa kufikia huduma ya uchunguzi na tiba.