Mustakhbali wa uchaguzi Bangladesh, tumieni mashauriano: Ban

11 Disemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina pamoja na Rais Abdul Hamid na kuwasihi wapatie suluhu tofauti zinazoibua ghasia nchini humo wakati huu wa kueleka uchaguzi wa wabunge mwezi Januari mwakani. Ghasia hizo zinazozidi kuenea tangu mwezi uliopita zimesababisha vifo.

Mazungumzo hayo yamefanyika wakati Naibu Mkuu wa ofisi ya siasa ndani ya Umoja wa Mataifa Fernandez Taranco akihitimisha ziara yake ya siku tano nchini Bangladesh ambapo katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dhaka maesema mzozo wa kisiasa nchini humo unagharimu maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambayo Bangladesh ilishayafikia.

Amesema wakati wa mazungumzo na viongozi wa nchi wameonyesha utaifa na sasa kilichobakia ni kupunguza mvutano na kuendelea kushiriki katika mashauriano ya dhati ili kuweka mazingira bora ya mwelekeo wa kisiasa.

Bwana Taranco ametaka pande zote zinazokinzana kuacha ghasia, viongozi wa upinzani waachiwe huru na maridhiano kuhusu ratiba ya uchaguzi.