Ni wakati wa watu ukanda wa Maziwa Makuu kufurahia amani: Bi Robinson

11 Disemba 2013

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukanda wa Maziwa Makuu, Bi Mary Robinson, amesema kuwa huu ndio wakati wa kutimiza ahadi zilizowekwa katika makubaliano ya amani, usalama na ushirikiano, ambayo yalisainiwa mjiini Addis Ababa mapema mwaka huu, ili watu wa ukanda wa Maziwa Makuu wapate kufurahia amani.

Bi Robinson amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York, mara tu baada ya kulihutubia Baraza la Usalama, ambalo limekutana kujadili hali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

“Tumejadili pia hali ya wakimbizi kwa ujumla, na pia hatua zinazochukuliwa kukabiliana na makundi mengine yenye silaha, na ujumbe niliotoa kwenye ziara yangu juzi ya ukanda ni kwamba sasa tunapaswa kuendeleza haraka mazungumzo ya kina chini ya utaratibu wa amani, usalama na ushirikiano, lakini pia kuwepo matunda ya amani kwa watu wa ukanda. Ni wakati wa watu kwenye ukanda huo kuhisi kuwa utaratibu huo unaleta mabadiliko katika maisha yao kupitia matunda ya amani.”

Bi Robinson amesema baada ya mkwamo wa mazungumzo ya Kampala ambapo makubaliano ya mwisho hayakutiwa saini, anataraji kuwa hapo kesho mjini Nairobi kutakuwa na mkataba ulotiwa saini na Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais Joyce Banda wa Malawi, ili kudondoa sehemu muhimu kutoka kwa makubaliano ya Kampala ambayo hayakutiwa saini.