Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu zaidi ya laki moja wamekufa mgogoro wa Syria ukifikisha siku 1000:UNHCR

Watu zaidi ya laki moja wamekufa mgogoro wa Syria ukifikisha siku 1000:UNHCR

Zikiwa zimetimia siku 1000 tangu mgogoro wa Syria uibuke inaelezwa zaidi ya watu laki moja wamekufa ikiwa ni wastani wa watu mia kwa siku huku wafanyakazi wa misaada na waandishi wa habari wakikabiliwa na vikwazo vya kuwafikia robo ya watu milioni walioko katika maeneo yaliyozingirwa na vikosi.

Hiyo ni kauli ya mjumbe maalum wa shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi UNHCR Angelina Jolie katika ujumbe wake wa kutimiza siku hizo ambapo amesisitiza kuwa dunia itaangalia nyuma kwa aibu kutokana na kushindwa kwa pamoja kuzuia vifo vya watu hao wasio na hatia.

Amesema hatua hii ya kutisha lazima ichochee kila mmoja anayehusishwa katika mazungumzo ya amani ya Geneva mwezi Januari ili kuukomesha mgogoro huo na kuhakiisha uhakika wa kufikisha misaada kwa watu waliotatizika nchini Syria.

Bi Jolie amesema kila siku maisha ya mamilioni ya wakimbizi wa Syria yanazidi kuwa magumu nusu yao wakiwa ni watoto na kuongeza kuwa anatumaini serikali na watu kote duniani watawahurumia na kupata hisia za kuwajibika kwa ajili yao ili kutoa misaada ambayo inahitajika zaidi. Amemaliza kwa kusema ni muhimu kwa jamii ya kimataifa kuhahkiisha siku nyingine 1000 za umwagajai damu nchini Syria zinakomeshwa.