Usajili wa watoto wachanga bado ni changamoto: Tanzania yachukua hatua: UNICEF

11 Disemba 2013

Wakati linatimiza miaka 67 tangu kuanzishwa kwake, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linasema usajili wa watoto wanapozaliwa umesalia tatizo kubwa duniani ambapo takwimu zinaonyesha kuwa watoto Milioni 230 duniani kote hawajasajiliwa popote.

Takwimu hizo zimo kwenye ripoti iliyotolewa leo wakati wa maadhimisho hayo iitwayo, Haki ya kila mtoto anayezaliwa: tofauti na mwelekeo wa usajili, ambayo inatumia takwimu zilizokusanywa kutoka nchi 161.

Akizungumzia ripoti hiyo katika mahojiano maalum na Diane Penn wa Radio ya Umoja wa Mataifa, mtaalamu wa takwimu kutoka UNICEF, Claudia Cappa amesema jambo hilo lina madhara makubwa kwani mtoto asiye na cheti cha kuzaliwa hawezi kupata haki zake za msingi ikiwemo elimu na afya.

 

"Ni muhimu pia kutambua kuwa usajili baada ya kuzaliwa na kupata cheti kunaonyesha umri wa mtoto. Na iwapo hawawezi kupata, hawawezi kuthibitisha wao ni watoto. Wanaweza kulazimishwa kuingia kwenye ndoa, kufanya kazi, kutumikishwa jeshini na hata kutendewa kama vile wao ni watu wazima. Na katika hali ya dharura, familia haiwezi kudai kuwa ina mtoto. Watoto wanaweza kusafirishwa kiharamu, na familia haiwezi kudai kuwa hao ni watoto wao.”

Ripoti hiyo pamoja  na kuweka bayana nchi 10 zenye viwango vya chini zaidi vya usajili wa watoto wanapozaliwa ikiwemoTanzaniaimesema nchi hiyo tayari imechukua hatua kushughulikia suala hilo.

Hatua hizo ni pamoja na kusogeza huduma za usajili karibu na wananchi na kuhakikisha usajili kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano ni bure, lakini pia simu za mkononi zinatumika kusafirisha takwimu za usajili.