FAO yataka usaidizi zaidi kwa kilimo cha milimani

11 Disemba 2013

Wakati dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya milima hii leo, Shirika la chakula la kilimo duniani, FAO limesema familia za wakulima zinazoishi kwenye milima na kando kando ya milima ni mtaji tosha unaoweza kuboresha hali ya usalama wa chakula na mazingira ya eneohilo.  George Njogopa na taarifa kamili

 (Ripoti ya George)

Kulingana na ripoti ya FAO  kiasi cha asilimia 40 ya wakazi wanaoishi maeneo ya milimani walioko katika nchi zinazoendelea wanakabiliwa na tatizo la usalama wa chakula. Kiwango hicho cha asilimia ni sawa na watu milioni 300 ambapo nusu yake wanaandamwa na matatizo sugu ya ukosefu wa chakula.Ripoti hiyo ya FAO iliyochapishwa leo kuambatana na siku ya Umoja wa Mataifa ya mlima imesema kuwa kuna haja ya kuwaangazia wananchi wanaishi kwenye maeneo ya milimani.

Katika kiwango cha dunia,milima inatajwa kuwa na usaidizi mkubwa ikitoa maji kwa nusu ya watu duniani.Ama wakulima wanaopatikana katika maeneo ya milimani wanelezwa kuwa ndiyo wanafanikisha shughuli nyingi za usaidizi wa mazingira.

Akizungumzia ripoti hiyo Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO kuhusu maliasili Maria Helena Semedo amesema siku ya milima duniani inamulika jinsi maliasili hiyo ilivyo muhimu kwa mustakhbali endelevu.

(Sauti ya Semedo)

Milima inatoa kati ya asilimia 60 hadi 80 ya maji safi kote duniani. Milima pia ina mchango mkubwa katika upatikanaji wa nishati safi. Milima inachangia usalama wa chakula na lishe, kwa kutoa ardhi ya kupanda mimea, malisho ya mifugo, maji ya kunapopatikana samaki na pia bidhaa za misitu kama matunda, vyoga na asali”