Guterres atoa ombi la kusaidia wakimbizi wa ndani:UNHCR

11 Disemba 2013

Kamishina mkuu wa wakimbizi Antonio Guterres leo amefungua mjadala wa kila mwaka wa changamoto za kulinda wakimbizi kwa ombi la kuimarisha mtazamo wa kimataifa kwa ajili ya watu takribani milioni 30 duniani ambao wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani nchini mwao.

Katika hotuba yake ya ufunguzi mjini Geneva bwana Guterres ameonya kwamba wakimbizi wa ndani wanaongezeka , ikiwa kuna ongezeko la asilimia 50 kwa miaka 15 iliyopita , huku kukiwa na dalili kwamba mwaka 2013 unaweza kuvunja rekodi kwa mamilioni ya watu zaidi kuwa wakimbizi wa ndani Syria na kwingineko.

Ameongeza kuwa anatiwa hofu na ukubwa watatizo hilo ambalo jumuiya ya kimataifa haijalipa uzito unaostahili, akisema kama lilivyo tatizo la wakimbizi wa kawaida, wakimbizi wa ndani mara nyingi hupata hifadhi kwa watu masikini au wasiojiweza maeneo ya vijijini ambako mara nyingi  wanakosa miundombinu ya kukabiliana na wimbi hilo, na pia inakuwa vigumu kuwafikia kwani maeneo hayo yanakuwa ni ya vita.

Shirika la wakimbizi UNHCR linasema hadi kufikia mwisho wa mwaka 2012 wakimbizi wa ndani milioni 17.7 wamekuwa chini ya uangalizi wa shirikahilo, baadhi ya sababu ni kwamba mfumo wa kisheria wa kimataifa haujaendelea vya kutosha kuweza kuwalinda na limeongeza kuwa hali hiyo pia inawakumba wakimbizi wengine.