Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikwazo dhidi ya mali za Taylor vyaendelezwa; Somalia yahitaji bado usaidizi

Vikwazo dhidi ya mali za Taylor vyaendelezwa; Somalia yahitaji bado usaidizi

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo kwa kauli moja limepitisha azimio linalokariri azimio lake la awali linalomzuia Rais wa zamani wa Liberia John Taylor, familia yake na maafisa waandamizi kutumia fedha walizozipata kinyume cha sheria wakati wa uongozi wake. Rais wa Baraza la usalama kwa mwezi huu wa Disemba, Balozi Gerard Araud wa Ufaransa aliweka mezani azimio hilo la leo namba 2128 la mwaka 2013 na baada ya kupiga kura akatangaza matokeo..

Anasema azimio limepitisha kwa kauli moja kwa wajumbe wote 15 kuunga mkono. Azimio hilo pia linataka miezi kumi na miwili baada ya kupitishwa hii leo, kuendeleza vikwazo vya usafiri kwa viongozi waandamizi wa iliyokuwa serikali ya Taylor pamoja na wake zao, pamoja na kuendeleza vikwazo vya silaha dhidi ya nchi hiyo.

Wakati huo huo, Baraza la Usalama limepokea taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusuSomaliaambapo mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini humo Balozi Nicholaus Kay alihutubia baraza kwa njia ya video kutoka mjiniMogadishu.

Bwana Kay amesema miezi mitatu tangu ahutubie barazahilo,Somaliaimekumbwa na matukio ikiwemo kura ya kutokuwa na imani na WAziri Mkuu, kujiuzulu kwa gavana wa Benki Kuu na hata mashambulio ya kigaidi.

(Sauti ya Balozi Kay)

“Kisichokuua kinafanya uwe thabiti zaidi. Majanga na mizozo yote iliyokumba Somalia katika miezi mitatu iliyopita hayafikii hata ya watabiri. Mzozo wa Benki Kuu utawezesha usimamizi mzuri wa taasisi za fedha. Kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu imekuwa ni jaribio kubwa kwa taasisi ya bunge na imekuta ziko thabiti.”

Amesema Umoja wa Mataifa umekuwa mstari wa mbele kusaidia ujenzi wa amani ya kudumu nchini humo ikiwemo kuhakikisha ratiba ya kuwa na serikali ya shirikisho na uchaguzi mwaka 2016 inazingatiwa. Bwana Kay akashukuru baraza la usalama kwa azimio la hivi karibuni la usaidizi kwa vikosi vya Afrika nchini humo, AMISOM.

(Sauti ya Balozi Kay)

“Nalishukuru baraza kwa usaidizi wao usiotetereka kwa kazi yetu Somalia. Itoshe kusema kuwa sote tuko katika maandalizi ya maisha bora. Somalia mpya inayoibuka inahitaji kuungwa mkono na sisi. Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono sauti za matumaini na si za kukata tamaa, fursa na siyo mizozo.”