Malkia Maxima na maafisa wa UM ziarani Ethiopia na Tanzania:

9 Disemba 2013

Malkia Máxima wa Uholanzi na Mashirika matatu ya chakula ya Umoja wa Mataifa wameungana kuelimisha jinsi fursa ya huduma za fedha kama kuwa na akaunti za benki, mikopo ya muda mfupi, mikopo midogomidogo, akiba na bima vinavyoweza kusaidia kuboresha maisha ya wakulima wadogowadogo na watu masikini vijijini.

Malkia Máxima ni mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masula ya kujumisha wote katika mfumo wa fedha kwa ajili ya maendeleo.

Leo Malkia huyo amewasili Addis Ababa Ethiopia katika mwanzo wa ziara ya siku tano nchini Ethiopia na Tanzania akiungana na Bi Ertharin Cousin Mkurugenzi mkuu wa shirika la mpango wa chakula WFP, Maria-Helena Semedo ambaye ni naibu mkurugenzi mkuu wa shirika la chakula na kilimo FAO, na Adolfo Brizzi, mkurugenzi wa sera na ushauri wa kiufundi katika mfuko wa kimataifa wa ufadhili wa maendeleo ya kilimo (IFAD).

Jumatano ujumbe huo unatarajiwa kusafiri kwenda Dar es Salaam, Tanzania, ambako utakuwepo hadi tarehe 13 December. Malkia Máxima na maafisa hao wa WFP, FAO na IFAD watakutana na maafisa wa serikali za Ethiopia na Tanzania , na viongozi wa mashirika ya fedha ya kitaifa na kimataifa. Katika ziara hiyo watakutana pia na viongozi wa jumia za vijijini na wakulima wadogowadogo ili kujadili jinsi gani kupanua wigo wa huduma za fedha kutawasaidia wakulima na kuwa tayari kukabiliana na majanga kama ukame na mafuriko kwa kuboresha uzalishaji.