Ban amsifu Mandela kama jabali wa haki na usawa

9 Disemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, ambaye yuko Afrika Kusini, amemsifu tena Hayati Mzee Nelson Mandela kama mtu aliyekuwa jabali wa haki, usawa na haki za binadamu. Akizungumza kwenye kituo cha ukumbusho cha Nelson Mandela, Bwana Ban amesema kuwa Nelson Mandela alikuwa zaidi ya mmoja wa viongozi wenye hadhi ya juu zaidi wa nyakati zetu, kwani alikuwa pia mwalimu ambaye alifundisha kwa kutoa mfano.

Bwana Ban amesema aluguswa sana na jinsi Mandela alivyotanguliza maslahi ya wengine, unyenyekevu wake na maadili yake. Amesema hiyo ni busara inayohitajika sasa, wakati zikifanywa juhudi za kuwasaidia watu walio katika hali dhoofu, vita vya silaha, kulinda haki za binadamu na kujenga ulimwengu bora zaidi, ambao Mandela alitolea mchango wake mkubwa.

Amesema kuwa watu wa Afrika Kusini na ulimwengu mzima umepoteza shujaa, na kwamba mfano wake utabakia daima, na kutoa mwongozo kwa kazi ya Umoja wa Mataifa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud