Zaidi ya watoto milioni 23 kuchanjwa dhidi ya ugonjwa wa polio mashariki ya kati

9 Disemba 2013

Zoezi kubwa zaidi la utoaji wa chanjo kuwahi kufanyika linaendela kwa sasa kwenye eneo la mashariki ya kati likiwa na lengo la kuwachanja  zaidi ya watoto milioni 23 dhidi ya ugonjwa wa polio nchini Syria na mataifa yaliyo jirani . Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Kampeni hiyo inajiri baada ya kutokea mkurupuko wa ugonjwa wa polio nchini Syria ambapo visa 17 tayari vimeripotiwa.

Ili  kuzuia kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo waandalizi wa zoezi hilo watatoa chanjo mfululizo kwa kipindi cha miezi kadha inayokuja kwa watoto wote walio chini ya miaka mitano wakiwemo walio nyumbani  au wale  waliolazimika kuhama kutokana na mizozo.

Ndani mwa Syria kampeni hiyo inalenga kuwafikia watoto milioni 2.2 wakiwemo wale waliokosa zoezi la kwanza. Asilimia kubwa ya watoto nchini Syria haifikiki hususana wale wanaoishi kwenye maeno yanayokumbwa na mizozo.

Kwa kipindi cha miezi kadha inayokuja UNICEF ina mipango kutoa chanjo milioni 10 za polio nchini Syria baada ya chanjo milioni mbili kuwasili mjini Damascus tarehe 29 mwezi uliopita.