Ban Kuhudhuria ibada ya kuomboleza kifo cha Mandela Jumanne

8 Disemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ataondoka mjini Paris Ufaransa kuelekea Afrika Kusini hapo kesho Jumapili, ili kuhudhuria ibada rasmi ya maombolezo ya Hayati Mzee Nelson Mandela, ambayo itafanyika mnamo siku ya Jumanne. Bwana Ban ambaye amekuwa Ufaransa kuhudhuria mkutano kuhusu amani Afrika, amesema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa kuna haja ya dharura ya kuepusha hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kuzidi kuzorota, na kutekeleza azimio la Baraza la Usalama liliopitishwa siku mbili zilizopita. Bwana Ban amezipongeza nchi zote zinazochangia vikosi kwa ujumbe wa kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati, MISCA, na kuisifu Ufaransa na Rais Hollande kwa kuwa msitari wa mbele katika kupeleka vikosi vyake CAR haraka, na hata katika kutoa uongozi kwenye Baraza la Usalama. Katibu Mkuu amesema kuwa katika mikutano yake yote na viongozi wa Afrika kwenye mkutano huo wa Elysee Ufaransa, amekuwa akisisitiza uhusiano baina ya amani, maendeleo na haki za binadamu, huku pia wakiangazia suala la mabadiliko ya tabianchi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter