Skip to main content

Ban ahudhuria mkutano wa amani Afrika, asema mizozo bado tatizo

Ban ahudhuria mkutano wa amani Afrika, asema mizozo bado tatizo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye yuko mjini Paris Ufaransa kuhudhuria mkutano wa siku mbili kuhusu amani na usalama barani Afrika amesema kuendelea kwa mizozo barani humo ni moja ya mambo ya kutazamwa.

Katibu Mkuu Ban amesema licha ya Umoja wa Mataifa kusaidia katika utatuzi wa migogoro lakini tishio la vikundi vyenye msimo mkali bado linatia hofu akitolea mfano nchini Mali ambako amesema kuna haja ya dharura ya majadiliano jumuishi yatakayoangazia kiini cha mgogoro.

Akizungumzia hali ya usalama nchini Somalia Bwana Ban amesema

(Sauti ya Ban)

Somalia imeunda upya taasisi za kitaifa na kuunda katiba ya muda ya shirikisho lakini maendeleo ya usalama yametatizika na hali ni tete. Msaada wa jumuiya ya kimataifa kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Somalia, AMISOM na mkakati mpya ni muhimu

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Ban amekutana na waziri mkuu wa Libya Ali Zeidan ambapo wamejadili hali ya usalama nchini humo na jukumu la ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia amani nchini Libya UNSMIL ikiwamo kuendelea kusaidia majadala wa kitaifa.

Katibu Mkuu Ban pia amekutana na rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo , DRC Joseph Kabila Kabarage ambapo viongozi hao wamejadili hali nchini DRC na ukanda wa maziwa makuu pamoja na mazungumzo ya amani ya Kampala. Bwana Ban alipongeza nchi hiyo kwa zoezi la mafanikio la kuvitimua vikosi vya waasi vya M23 na kusisitiza kuwa ushindi wa kijeshi hautatatua tatizo la M23 na kuongeza kuwa ni vyema mzozoz huo ukatatauliwa kisiasa.

Ban kadhalika amesisitiza umuhimu wa kushughulikia vikundi vingine vya kijeshi amabvyo vinatishia usalama wa wananchi huko Mashariki mwa DRC huku akiitaka nchi hiyo kuendeleza mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.