Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mandela alifuata maadili kuliko kiongozi yeyote wa zama za sasa: Pillay

Mandela alifuata maadili kuliko kiongozi yeyote wa zama za sasa: Pillay

Mzee Madiba , Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini Nelson Mandela aliyeaga dunia Alhamisi anatambulika kama kinara wa uhuru, usawa na haki za binadamu. Hayo yamesemwa na Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa Navi Pillay aliyeongeza kuwa Mandela pengine ndiye kiongozi mfuata maadili kuliko mwingine yeyote katika kizazi hiki.

Amesema aliamini katika haki za binadamu kwa wote, alichagiza haki za wanawake, usawa katika ya wanawake na wanaume na kuwawezesha wanawake katika madaraka. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu

(SAUTI YA RUPERT COLVILLE)

Licha ya kukaa jela miaka 27 hakufuata njia ya kulipiza kisasi. Kamishina mkuu anakumbuka vyema hatimaye alipoachiliwa huru hamasa iliyokuwepo nchini Afrika ya Kusini ilikuwa ya aina yake, hisia za chuki, kiu ya kulipiza kisasi, hamu ya kuwabagua waliofanya hivyo dhidi waio weupe. Amesema naye alikuwa na hisia kama hizo, kwani ni vigumu kutokuwa nazo, baada ya miaka mingi ya kuishi chini ya ubaguzi wa rangi, lakini Mandela alikataa kufuata njia hiyo, kama alivyokataa muafaka wowote wa kumuachilia kwa malipo ya kuuza misingi ya ukombozi. Alibadili yote kwa kauli tu, aliwaambia Waafrika Kusini kurusha mishale na silaha zao baharini. Aliwaambia kuweka kando hamu ya kulipiza kisasi na kuifanyia kazi afrika ya Kusini ambayo sio tuu huru bila ubaguzi wa rangi bali huru kutokana na mifumo yote ya ubaguzi., Aliwaonyesha kwamba mustakhbali mzuri unategemea maridhiano na sio kisasi.”