Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lapitisha azimio la kuruhusu vikosi vya kurejesha utulivu CAR

Baraza la Usalama lapitisha azimio la kuruhusu vikosi vya kurejesha utulivu CAR

Wakati hali tete ikiwa imetanda kwenye mji mkuu wa Bangui katika Jamhuri ya Aftrika ya Kati kufuatia shambulizi lililosababisha vifo vya raia, Baraza la Usalama limechukuwa hatua mathubuti kurejesha utulivu nchini humo. Joshua Mmali na taarifa kamili.

(TAARIFA YA JOSHUA)

Katika azimio lililoungwa mkono na kupitishwa kwa kauli moja, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,  linatoa uungwaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa vikosi vya Muungano wa Afrika vya kurejesha utulivu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, MISCA.

MISCA pia inapewa idhini chini ya aya ya saba ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na hivyo kuiruhusu kufanya operesheni zake katika kuwalinda raia. Umoja wa Mataifa pia utasimamia hazina ya kuratibu michango ya kifedha kwa kuunga mkono vikosi vya Afrika.

Mengine yaliyomo katika azimiohilo, yamesomwa na Mwakilishi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, Gérard Araud

“Pili, azimio linadhinisha vikosi vya Ufaransa kusaidia vikosi vya Afrika, MISCA katika kutekeleza majukumu yake. Tatu, azimio linaandaa hatua zitakazofuata. Linauomba Umoja wa Mataifa kujiandaa sasa uwezekano wa kubadili vikosi vya Afrika kuwa ujumbe wa Umoja wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa. Azimio pia linaangazia kukabiliana na ukiukwaji wa haki za binadamu, linaweka tume ya uchunguzi, pamoja na kuandaa msingi wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa.”

Mapema asubuhi, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Babacar Gaye, na wawakilishi wengine wa kimataifa wamelaani vikali shambulizi lililosababisha vifo kadhaa mapema leo katika mji mkuu wa Bangui, na kutoa wito kwa mamlaka za CAR kutimiza wajibu wao na kukomesha mara moja  mapigano na kurejesha utulivu, na pia kwa raia kujiepusha na vitendo vya ulipizaji kisasi.