Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko jopo la UM-OPCW kwa kazi inayoendelea Syria: Baraza la usalama

Heko jopo la UM-OPCW kwa kazi inayoendelea Syria: Baraza la usalama

Wajumbe wa baraza la usalama leo wamepatiwa ripoti ya pili ya kila mwezi kutoka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uchunguzi wa silaha za kemikali nchini Syria.

Ripoti hiyo iliwasilishwa kwenye kikao cha faragha na mratibu maalum wa ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na OPCW Sigrid Kaag kwa mujibu wa azimio namba 2118.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Disemba Balozi Gerad Araud wa Ufaransa amesema wajumbe wamesifu kazi nzuri inayofanwya na jopohilokatika mazingira magumu. Kuhusu awamu ya kwanza ya utekelezaji wa azimio 2118 amesema inaendelea vizuri lakini kuna changamoto mbili.

 (Sauti ya Balozi Araud)

 “Kwanza ni usafirishaji wa kemikali husika kwenda bandari ya Latakia na kila kitu kinategemea hali ya usalama barabarani ambayo bado inatia hofu kutokana na mapigano huko Syria. Na pili ni usafirishaji wa kemikali hizo nje ya nchi hiyo na kuziteketeza. Nafikiri sasa mwelekeo wetu ni kwa awamu hizo kwa miezi ijayo.”

Naye Bi. Kaag alisema kazi inaendelea vizuri  na maaandalizi sasa ni kwa awamu ya tatu ya kuondoa kemikali husika kutoka nje ya nchi hiyo. Changamoto ni pamoja na kuhakikisha wanazingatia muda uliowekwa, wanafanya kazi kwa ufasaha lakini usalama bado ni tatizo..

 (Sauti ya Kaag)

“Mfano ni barabara inayounganisha Damascus na Homs, ni njia kuu na iwapo hatuwezi kuitumia ni tatizo kubwa. Nililazimika kusafiri kwenda Latkia kupitia Lebanon  kwa kutumia helikopta kuhakikisha nimefika bandarini kujadiliana na maafisa husika. Kwa hiyo kuna matatizo na mambo ambayo yako nje ya uwezo wetu.”