Kuna unafuu Sudan Kusini, lakini tuongeze juhudi:Kang

4 Disemba 2013

Naibu Mkuu wa ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu ndani ya Umoja wa Mataifa, OCHA, Kyung-wha Kang, amezungumza na waandishi wa habari mjini New York na kuwaeleza kile alichoshuhudia wakati wa ziara yake Sudan Kusini ikiwemo kuimarika kidogo kwa hali ya kibinadamu nchini humo lakini bado Umoja wa Mataifa na wadau wake unaendelea kutoa usaidizi.

Amesema wakazi wa Jonglei na Juba walimweleza machungu wanayopitia baada ya kupoteza makazi, mali na hata jamaa zao kwenye mizozo ya mara kwa mara na ndipo alipofanya mazungumzo na viongozi wa maeneo hayo ilikuwa dhahiri kuwa hatua zaidi zapaswa kuchukuliwa..

(Sauti ya Kyung-Wha)

“Kwenye mashauriano yangu na viongozi wa huko Jonglei na mji mkuu Juba, tulizingatia  umuhimu wa kupatia suluhu ya kudumu mzozo huo wa muda mrefu nchini Sudan Kusini kwa kuwekeza katika mifumo bora ya kushughulikia majanga, kuimarisha miundombinu muhimu ya nchi hiyo na kuhakikisha kuna amani ya kudumu.”

Alipoulizwa kuhusu ujio wa raia wa Sudan Kusini kutoka Sudan, Naibu Mkuu huyo wa OCHA alisema kuna raia Milioni Moja nukta Tisa wanaotaka kurejea na wasiwasi ni kwa wale Elfu Ishirini na watatu walioko mji mkuu wa Sudan, Khartoum ambao makazi yao ni dhalili.

Hata hivyo Bi. Kang amesema kuna wengine wanaendelea kurejea kwa usaidizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi, UNHCR na lile la kimataifa la uhamiaji, IOM.