UN Women yaangazia iwapo Malengo ya Milenia yamenufaisha wanawake na wasichana

4 Disemba 2013

Mkutano wa siku mbili kuhusu changamoto na ufanisi ulofikiwa katika kufikia malengo ya maendeleo ya milenia kuhusu wanawake na watoto wa kike, umeanza leo mjni New York, ukiwa umeandaliwa na kitengo kinachohusika na m asuala ya wanawake katika Umoja wa Mataifa, UN Women. Joshua Mmali na taarifa kamili

(TAARIFA YA JOSHUA)

Mkutano huo, kulingana na UN Women, unalenga kuweka msingi wa kongamano la 58 la kamisheni kuhusu hali ya wanawake, ambalo litafanyika mnamo mwezi Machi mwaka 2014.

Akihutubia kikao cha ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UN Women, Bi Lakshimi Puri amesema kuja kwao pamoja na muhimu katika kuunganisha juhudi za kuongeza kasi ya kutekeleza malengo ya maendeleo ya milenia kwa wanawake na watoto wa kike.

Tunapokaribia tarehe ya ukomo wa MDGs ya 2015, ni wakati wa kuweka msukumo wa mwisho kuongeza kasi ya utekelezaji. Ni wakati wa kufanya tathmini, siyo tu kwa kukagua kilichofanyika, bali pia kwa kutizama mbele na kuweka barabara ya siku zijazo.”

Mkutano huo ambao unawaleta pamoja wadau wote katika masuala ya haki za wanawake, unatazamia pia kutoa nafasi ya kuongeza uelewa kuhusu ahadi zilizopo, kufundishana kutokana na vilivyotimizwa na mikakati ilowekwa, pamoja na kuendeleza mashauriano.

Bi Puri amesema, kutimiza mabadiliko halisi na ya kudumu katika maisha ya wanawake na watoto wa kike, kunahitaji kuzingatia misingi ya kutokuwepo usawa wa kijinsia.